Monday, April 30, 2012

AND 1 ya Marekani yang’ara katika mpira wa kikapu

Na Mwandishi wetu
Timu ya mpira wa kikapu inayoundwa na wachezaji nyota wa zamani wa ligi ya Chama mpira wa kikapu cha Marekani American Basketball Association (ABA)  ijulikanayo kwa jina la AND1 imemaliza ziara yake kwa mafanikio makubwa huku ikiacha somo na gumzo kwa Watanzania kutokana na ujuzi walionyesha katika mchezo huo.

Andi 1 iliyokuwa chini ya mchezaji nyota, Dennis Chism maarufu kwa jina la Spyda iliweza kufanya mambo makubwa mkoani Mwanza na Arusha baadaye jijini Dar es Salaam na kuitandika Dar Dream team kwa 123-71.

Mbali ya Spyda, wachezaji wengine waliokuwepo katika ziara hiyo ni Phillip Champion Hotsauce, Robert Martin, Marvin Collins Highrizer, Brandon LaCue Werm, Jamar Davis, Alonzo Miles, Paul Otim na Justin Darlington.

Chism akipaa hewani kufunga dhidi ya Dar es Salaam

Chism alisema pamoja na kuwashukuru wauzaji wa kinywaji cha Sprite kwa udhamini wao na kufanikisha kuja nchini, wamefuraishwa na jinsi wachezaji wa Tanzania waliovyoonyesha vipaji vyao. Alisema kuwa wachezaji hao wanatakiwa kuendelezwa ili kufikia hatua kubwa na hata kuweza kucheza ligi za kikapu za kulipwa Duniani pamoja na ile ya NBA.

Mbali ya kucheza, wachezaji hao walionyesha vipaji mbali mbali walivyonavyo katika kufunga pointi tatu, ku-dank na staili nyingine ambazo ziliwasisimua mashabiki wengi.

hapa And 1 wakifunga dhidi ya Arusha

Baada ya kushiriki katika mechi za mpira wa kikapu, wachezaji hao walijumuika na watanzania wengine katika tamasha la muziki la Coca Cola A Billion Reasons to Believe  lililofanyika kwenye  ufukwe wa Mbalamwezi na kuona jinsi gani watanzania walivyokuwa wataalam katika muziki wa kizazi kipya na hip hop ambao asili yake ni Marekani ambako wao ndiyo maskani yao.

hapa Chism akisaini katika daftari la wanafunzi mkoani Mwanza baada ya kuvutiwa na uchezaji wake.
Wakali wa muziki kama Ambwena Yesaya (AY) na Nemeless kutoka Kenya walitamba katika tamasha hilo lililofana na kuwavutia mashabiki wengi.

AY akifanya vitu vyake katika tamasha la Coca Cola a Billion Reason to Believe

AY akifanya vitu vyake mbele ya mashabiki katika tamasha la Coca Cola a Billion Reason to Believe
Nemeless akifanya vitu vyake mbele ya mashabiki

And 1 nao walikuwepo katika tamasha hilo

Sunday, April 29, 2012

Chelsea yaua England

Mshambuliaji wa Chelsea, Fernando Torres (kulia) na mabeki wa Queens Park Rangers, Anton Ferdinand (katikati) na Shaun Derry (kushoto), wakiwania mpira wakati wa mechi ya Ligi Kuu England iliyopigwa Uwanja wa Stamford Bridge jijini London, England leo.


LONDON, England
Fernando Torres alirejesha makali yake baada ya kufunga mabao matatu katika ushindi wa mabao 6-1, dhidi ya QPR.

Daniel Sturridge aliifungia Chelsea bao la kwanza sekunde ya 45, kabla ya John Terry kuongeza bao la pili, Torres alikwamisha mabao matatu na  Florent Malouda bao moja, wakati Djibril Cisse aliifungia QPR bao lao.

Simba kweli kiboko ya waarabu

Milovan

WAWAKILISHI pekee katika michuano ya kimataifa nchini, Simba, jana waliibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Al Shady ya Sudan, katika mechi ya Kombe la Shirikisho Afrika iliyochezwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Kwa matokeo hayo, Simba wamejiweka katika nafasi nzuri ya kusonga mbele katika michuano hiyo, ikiwa watafanikiwa kulinda ushindi wao ugegeni wiki mbili zijazo, sare ya aina yoyote ama kufungwa mabao yasiyozidi mawili.

Simba ambao ni wenyeji katika mechi hiyo, walianza mchezo kwa kasi na kulifikia lango la wapinzani wao, lakini Felix Sunzu alipokea mpira kutoka kwa Emmanuel Okwi na kupiga shuti kali lililopaa juu ya lango.

Al Shady ilijibu mashambulizi hayo dakika ya 19, baada ya Nadir Eltaueb kupiga shuti la mbali lililokuwa likielekea wavuni, lakini kipa wa Simba, Juma Kaseja alilipangua na kuwa kona ambayo haikuzaa matunda.

Simba katika dakika ya 37, walipata penalti baada ya kipa wa Al Shady, Abdelrahman Ali kumkamata Okwi aliyekuwa akielekea kuzitisa nyavu zao, lakini Patrick Mafisango alikosa bao.

Wawakilishi hao wa Tanzania walirekebisha makosa yao dakika 66, baada ya Haruna Moshi 'Boban' kuifungia bao la kwanza timu yake akitumia vizuri pasi iliyotoka kwa Mzambia Felix Sunzu.

Baada ya kukosa penalti, Patrick Mafisango alisahihisha makosa yake kwa kuipatia timu yake bao la pili dakika ya 87, akitumia vizuri mpira uliotoka kwa Okwi.

Okwi aliyekuwa akiisumbua sana ngome ya wapinzani wao, alifanikiwa kufunga bao la tatu dakika ya 88, akitumia vizuri mpira uliotoka kwa Sunzu na kuukwamisha wavuni.

Simba italazimika kusafiri mpaka Sudan wiki mbili zijazo kurudiana na Al Shady.

Simba: Juma Kaseja, Nassoro Masoud, Amir Maftah, Shomari Kapombe, Kelvin Yondan, Patrick Mafisango, Uhuru Seleman, Mwinyi Kazimoto, Felix Sunzu, Haruna Moshi 'Boban', Emmanuel Okwi.

Al Shady: Abdelrahman Ali, Elnour Altigani, Issac Seun Malikh, Sadam Abu Talib, Fareed Mohamed,  Zakaria Nasu, Razak Yakubu, Faris Abdalla, Hamouda Bashir, Nadir Eltaueb, Bassiro Ubamba.

Simba mwacheni aitwe Simba, yaigagadua Al- Shandy ya Sudan 3-0


 Mchezaji wa timu ya Simba Mganda Emmanuel Okwi akikokota mpira kuelekea goli la timu ya Al Ahly Shandy, huku mchezaji wa timu ya Isaac Seun Malik wa timu ya Al- Shandy ya Sudan akijaribu kumzuia katika mchezo wa kombe la Shirikisho unaofanyika kwenye uwanja wa taifa jijini Dar es salaam hivi sasa ni kipindi cha pili na hakuna timu iliyokwishaona lango la mwenzake.
 Timu zikiingia uwanjani kabla ya mchezo huo kuanza jioni hii.
 Mashabiki wa Simba wakishangilia huku wakiwa wameshika sanamui ya Simba
 Kundi la ushangiliaji la Mpira Pesa kutoka Magomeni likishangilia kwa nguvu

MAUGO ASHIKISHWA ADABU NA CHEKA


BONDIA Francis Cheka ‘SMG’ kutoka Morogoro, kwa mara ya tatu mfululizo Jana Usiku amempiga mpinzani wake Mada Maugo kwa Technical Knockout (TKO) raundi ya saba katika pambano lililokuwa la raundi 12, kwenye ukumbi wa PTA, Saba Saba, Dar es Salaam.
Maugo baada ya kupigwa ngumi nyingi katika raundi tatu mfululizo, kiasi cha kutabiriwa kukaa chini wakati wowote, mwanzoni mwa raundi ya saba hakurejea ulingoni.
Msaidizi wake, Karama Nyilawila alitupa taulo ulingoni akisema bondia wake hataendelea na pambano.
Refa John Shipanuka kutoka Zambia aliyelimudu pambano hilo, alimuinua mkono Cheka kumtangaza mshindi kwa TKO raundi ya saba.
Baada ya hapo, Maugo aliinuka kwenye kona yake na kwenda kumkumbatia Cheka na kocha wake, akisema kwamba amesalimu amri baada ya kuishiwa pumzi.
“Pumzi imekata, siwezi kuendelea,”alisema Maugo ambaye leo alionekana muungwana ingawa hakuwa tayari kusema atahitaji pambano la nne au la.
Akiwa mwenye furaha, Cheka alisema kwamba anamshukuru Mungu amemuwezesha kuendeleza ubabe wake kwa mabondia wa Tanzania na sasa anageuzia makali yake kwa Japhet Kaseba ambaye naye ameomba pambano la marudiano.
Katika pambano la jana, refa Shipanuka alimdhibitu Maugo mwenye desturi ya kuwakumbatia wapinzani wake ili kukwepa kupigwa na pia kupumzikia kwenye miili yao.
Kila alipokuwa akimkumbatia Cheka, Shipanuka alikuwa akifika na kuwaachanisha na kufanya mabondia hao watumie muda mwingi kupigana.
Pamoja na hayo, Maugo alilianza pambano hilo vizuri na katika raundi ya pili almanusra ashinde kwa Knockout (KO) baada ya kumkalisha mpinzani wake kwa ngumi kali.
Lakini SMG aliinuka na kuendelea na pambano, ingawa limchukua hadi raundi ya nne kuanza kuutawala mchezo.
Raundi ya kwanza hadi ya tatu, Maugo alifanya vizuri, lakini baada ya hapo mambo yalikuwa magumu na tangu hapo wengi walijua angepigwa wakati wowote.
Katika  mapambano ya utangulizi, mdogo wake Cheka, Cosmass Cheka alipigwa kwa pointi na Sadiki Momba katika pambano la uzito wa Light, wakati Hajji Juma alimpiga kwa pointi Emmilio Naffat uzito wa bantam.
Simba Watunduru alimpiga kwa KO raundi ya sita Mohamed Kashinde katika pambano la uzito wa Feather, wakati Amos Mwamakala alimpiga kwa pointi Said Muhiddin uzito wa Light.

Moro Best alimpiga Nassib Ramadhan kwa TKO raundi ya nne uzito wa Bantam na Salima Kabombora alimpiga Asha Ngedere kwa pointi uzito wa Bantam.

Cheka alivyomcheka Maugo jana

Baadhi ya Marefarii kutoka Nnje ya nchi wakisubili kuchezasha mpambano wa ubingwa wa IBF Arika kati ya Mada Maugo na Francis Cheka jana.
Baadhi ya mashabiki waliokuwa wamekaa katika VIP wakiangalia mpambano
Mada maugo kushoto na Francis Cheka wakioneshana umwamba wa kutupiana masumbwi

Cheka akipiga ngumi bila mafanikio uku mada akiludi nyuma kujiami.
Meya wa Manspaa ya Ilala Jery Slaa akimkabidhi funguo ya gari bondia Francis Cheka baada ya kuibuka na ubingwa wa k.o raundi ya 6 jana.

NCHUNGA AUNGURUMA JANGWANI, AWAPASHA WAZEE, AMTIMUA SEIF MAGARI

Lloyd Nchunga (kushoto) na Louis Sendeu
 
 
MWENYEKITI wa Yanga, Wakili Lloyd Baharagu Nchunga amejibu mapigo ya Baraza la Wazee la klabu hiyo, waliotaka kuichukua timu kufuatia mgogoro unaoendelea klabuni.
 
Lakini Nchunga amekataa ombi au taarifa ya kujiuzulu kwa Mjumbe wa Kamati ya Usajili na Kamati ya Mashindano, Abdallah Ahmed Bin Kleb, wakati huo huo akimkubalia Mjumbe wa Kamati ya Utendaji, Seif Ahmad Magari kuachia ngazi.
 
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari asubuhi ya leo, makao makuu ya klabu makutano ya mitaa ya Twiga na Jangwani, Dar es Salaam, Wakili Nchunga alisema kwamba Kamati ya Utendaji katika kikao chake cha jana imekubali kujiuzulu kwa Seif, lakini imekataa kwa Bin Kleb.
 
Aidha, kuhusu Wazee kuchukua timu, Nchunga alisema kweli alifanya nao kikao ana akawaambia atakuwa tayari kuwaachia timu waihudumie kwa mujibu wa Katiba, lakini kwanza lazima watoe vielelezo juu ya vyanzo vyao fedha ili ajue uhalali wake, wasije wakaiingiza klabu kwenye matatizo. 
 
Alisema anahofia wasije wakawa wanapata fedha kutoka kwa watu wenye kufanya biashara haramu ya dawa za kulevya- wakaiingiza Yanga kwenye matatizo.
 
Nchunga alisema iwapo watamuhakikishia vyanzo halali vya mapato, kwa mujibu wa Katiba atawaachia jukumu la kuihudumia timu na si kuhodhi madaraka ya uongozi.
 
Kwa kuwa Wazee walitaka kuanzia kazi kwenye mechi dhidi ya Simba Mei 5, mwaka huu, maana yake wao watahudumia timu, lakini mapato ya mechi watachukua akina Nchunga. 
 
Baada ya kuifunga JKT Oljoro 4-1 wiki hii, wachezaji wa Yanga walipewa mapumziko na jana walikusanyika tayari kuanza mazoezi, ingawa walikwama kwa sababu ya mvua.
 
Mwenyekiti wa Yanga, Nchunga amesema timu sasa itaingia kambini kesho na kuanza mazoezi moja kwa moja chini ya makocha Fred Felix Minziro na Salvatory Edward, wakati huo akisikilizia Wazee kama watatekeleza masharti yake awakabidhi timu.

Saturday, April 28, 2012

WAZEE YANGA WATEKA TIMU, NCHUNGA ANALO MWAKA HUU


Katibu Mkuu wa Baraza la Wazee la YANGA, Mzee Ibrahimu Akilimali (katikati) akizungumza na Waandishi wa Habari.

BARAZA la Wazee la klabu ya Yanga ya Dar es Salaam imeamua kuichukua timu ili kuiandaa na mechi dhidi ya wapinzani wao wa jadi, Simba SC Mei 5, mwaka huu kufuatia mgogoro unaoendelea klabuni.
 
Asubuhi ya leo, wazee wa Yanga wakiongozwa na Katibu wao Mkuu, Ibrahim Ally Akilimali walifika makuu ya klabu, makutano ya mita ya Twiga na Jangwani, Dar es Salaam na kufanya  Mkutano na Waandishi wa Habari.
 
Katika Mkutano huo, Mzee Akilimali alisema maamuzi hayo yana Baraka za Mwenyekiti wa klabu, Wakili Lloyd Baharagu Nchunga.
 
Kwa sasa Yanga ipo katika mgogoro, kufuatia Wajumbe wake wawili wa Kamati ya Mashindano na Usajili, Abdallah Ahmed Bin Kleb kujiuzulu kwa kutoridhishwa na mwenendo wa uongozi.
 
Machi mwaka jana, aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Davis Mosha naye alijiuzulu kwa sababu za kutoelewana na Mwenyekiti wake, Nchunga.
Yanga iliyopoteza matumaini hata ya kushika nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu, inaingia kwenye mechi dhidi ya watani wa wa jadi, Simba walio katika hali nzuri.
 
Kwanza wana uhakika wa kuchukua ubingwa na pili wanaendelea vizuri kwenye michuano ya Afrika, kesho wakicheza mechi ya kwanza ya hatua ya 16 Bora ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Al Ahly Shandy ya Sudan. 

(Kwa hisani ya BIN ZUBEIRY)

Wednesday, April 25, 2012

Twanga yamnyakua mpiga tumba Mapacha Watatu

Salehe Waziri 'Salehe Tumba' akipiga tumba
BENDI ya muziki wa dansi ya African Stars 'Twanga Pepeta' imemnyakua mpiga tumba wa bendi ya Mapacha Watatu, Salehe Waziri maarufu kama 'Salehe Tumba' kuziba pengo la Said Mohammed 'MCD' aliyetimkia Mashujaa.

Akizungumza Dar es Salaam leo, Mkurugenzi wa African Stars Entertainment Tanzania (ASET) inayomiliki bendi ya Twanga Pepeta, Asha Baraka, amesema hatua ya kumnyakua mpiga tumba huyo ni kuimarisha bendi yake.

" Tayari tumekwishakamilisha taratibu za makubaliano na  mwanamuziki huyo na tumesaini naye mkataba wa miaka mitatu leo," amesema Baraka.

Amesema Waziri ataungana na Badi Bakule aliyejiunga na bendi hiyo hivi karibuni akitokea Levent Musica ya Morogoro, na akawaomba mashabiki wa bendi yake wakae mkao wa kuendelea kupata burudani safi kutoka kwa bendi hiyo ambayo ni 'kisima cha burudani'.

Mkurugenzi huyo amesema Waziri aliyewahi kupigia bendi dada ya zamani ya Twanga Pepeta, Chipolopolo, ataungana na mpiga tumba mwingine, Kaboshoo huku akishirikiana na wapiga vyombo wengine, Miraji Shakashia 'Shakazulu', James Kibosho, Jumanne Mkandu 'Jojoo', Godfrey Kanuti, Victor Mkambi na Selemani Shaibu.

Pia, anaungana na wanenguaji, Abdillahi Zungu, Kassim Mohammed 'Super K', Bakari Kisongo 'Mandela' Said Mtanga, Fasha Sunday, Beatrice Mwangosi 'Baby Tall', Asha Said 'Sharapova', Mary Khamis, Vicky Pandapanda, Sabrina Mathew na Maria Soloma.

Baadhi  ya waimbaji ni Saleh Kupaza, Mwinjuma Muumini, Ramadhani Athumani 'Dogo Rama', Luiza Mbutu, Msafiri Said 'Diouf', Jumanne Said, Khamis Amigolas, Venance Mgori, Haji Ramadhan, Hadija Mnoga 'Kimobitel', Janeth Isinika.

Amesema hivi sasa wanajiandaa kuingia studio kwa ajili ya kurekodi wimbo wao mpya wa Shamba la Twanga uliotungwa na Grayson Semsekwa na pia kurekodi video za wimbo huo na nyingine mpya.

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI


NDUGU waandishi.

Kama mnavyofahamu, Jumapili ya Aprili 29 mwaka huu, timu ya soka ya Simba inakutana na klabu ya Al Ahly Shandy kutoka Sudan katika mchezo wa hatua ya 16 bora ya michuano ya Kombe la Shirikisho (CAF), kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Simba ni timu pekee kutoka katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) iliyobaki katika michuano yote ya kimataifa inayosimamiwa na CAF.

Kubwa zaidi, ndiyo wawakilishi pekee wa Tanzania waliobaki katika michuano ya kimataifa na hivyo wanabeba bendera ya taifa kokote kule waliko.

Maandalizi yote kwa ajili ya pambano hilo yamekamilika.

Wapinzani wetu, Al Ahly wanatarajiwa kuwasili kesho saa saba mchana kwa ndege ya Ethiopia Airlines.

Waamuzi na Kamishina wa mchezo wamepangwa kuwasili Ijumaa (keshokutwa) wakitokea nchini Swaziland na Rwanda.

VIINGILIO

Kutokana na ukweli kwamba mechi hiyo itakuwa ya kimataifa, Simba imepanga viingilio ambavyo kila mwananchi ataweza kuvimudu. Viingilio vitakuwa kama ifuatavyo.

Viti vya bluu na kijani itakuwa Sh. 5,000, Rangi ya Chungwa Sh, 10,000, VIP C 15,000, VIP B 20,000 na VIP A 30,000.

Tiketi zitauzwa katika maeneo yafuatayo, Big Bon, Benjamin Mkapa, Stears Mjini, Mbagala Dar Live, OilCom Buguruni, Tandika Mwembeyanga, Ubungo Oilcom, Mwenge Bus Stand, BP Mwananyamala na Gapco Ukonga.

Tiketi zitaanza kuuzwa siku ya Ijumaa asubuhi katika maeneo yaliyotajwa.

Klabu imepokea maombi mengi kutoka kwa wanachama na wapenzi wake kutoka mikoani na ingeomba kwamba wale wanaotaka kuja kutazama mechi hii kwa makundi kutoka mikoani, wawasiliane mapema na uongozi ili wanunuliwe tiketi zao mapema.

Simba SC imechapa tiketi za kutosha na ingeomba wapenzi na wanachama wake kujitokeza kwa wingi kwenye pambano hilo.

Wana Simba wote wanaombwa kuja uwanjani wakiwa wamevalia mavazi yao ya rangi Nyekundu na Nyeupe ili uwanja mzima upendeze kwa rangi hizo.

Tunatoa wito kwa vyombo vya habari kuisaidia Simba na Tanzania kwa kuelekeza nguvu zao katika uandishi wa taarifa ambazo zitaisaidia timu yetu kusonga mbele na si kuondoa morali au kusababisha watu wasiende uwanjani.

Shukrani.

Uongozi wa Simba SC unatoa shukrani, kwa namna ya kipekee kabisa, kwa serikali kutokana na uamuzi wake wa kuruhusu Wekundu wa Msimbazi kufanya mazoezi katika Uwanja wa Taifa kujiandaa na mechi hii muhimu.

Ezekiel Kamwaga
Msemaji
Simba SC

Chelsea raha tupu, yaitupa nje Barcelona

Mshambuliaji wa Barcelona, Lionel Messi (kulia) na Branislav Ivanovic.

BARCELONA, Hispania
CHELSEA , imekata tiketi ya kucheza fainali ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya kwa kuifunga jumla ya mabao 3-2 Barcelona, ingawa nahodha wake John Terry alitolewa nje kwa kuoneshwa kadi nyekundu.

Chelsea 'Blues' walikuwa katika wakati mgumu baada ya bao lililofungwa na Sergio Busquets na Andres Iniesta kuiongezea bao la pili Barca, pamoja na kutolewa nje Terry kwa mchezo mbaya.

Lakini, Ramires alirejesha matumaini kwa kuifungia Chelsea bao la ugenini.

Lionel Messi alishindwa kufunga mpira wa penalti baada ya shuti lake kugonga mwamba wa juu, kabla ya Fernando Torres aliyeingia dakika ya 80 kuchukua nafasi ya Didier Drogba kuifungia bao la pili timu yake dakika ya 90.

Mapema wiki hii, Torres alisema "timu bora haiwezi kushinda siku zote" . Maneno yake kama yalikuwa utabiri kwa mshambuliaji huyo aliyewazidi mbio mabeki wa Barca na kuipeleka Chelsea katika fainali zitakazopigwa mjini Munich Mei 19, mwaka huu.

Ndivyo alivyofunga goli hilo, Torres ambaye alikuwa na wakati mgumu wa kutikisa nyavu tangu alipojiunga na Stamford Bridge na kupata sifa vijana wa Roberto di Matteo usiku wa kuamkia jana.

Barcelona msimu huu umetikisa nyavu mara 102 kwenye Uwanja wa Nou Camp na mabao 18 yakufungwa , ikiwa mechi za klabu  bingwa za nyumbani.

Chelsea, katika mechi nne zilizopita imecheza bila ya kufungwa, ikiwemo iliyopigwa Nou Camp mjini Barcelona, kwa kufanikiwa kutoa sare ya mabao 2-2.

Lionel Messi ameendelea kuwa bila bao katika mechi zote mbili dhidi ya Chelsea, ambapo Fernando Torres anakuwa mchezaji wa 19, kuweka historia katika michuano hiyo dhidi ya Real Madrid na Barca. Ni mara ya kwanza kwa Mhispania kufanya hivyo.

Ingawa, Chelsea katika mechi zake tatu za Nou Camp, ilifanikiwa kutoka sare, wakati Real Madrid iliichapa Barcelona Jumamosi, na Blues walikuwa wakiongoza bao 1-0, waliyoshinda mechi ya kwanza, bao lililofungwa na Didier Drogba'.

Ajabu, mabao yote matatu ya Chelsea katika michuano hiyo, yalifungwa dakika za mwisho.
Kikosi hicho cha Chelsea katika mechi ya fainali itakayopigwa mjini Munich kitawakosa Ramires, Terry, Branislav Ivanovic na Raul Meireles.

Barcelona: Valdes, Pique/Alves, Puyol, Fabregas/Keita, Xavi, Iniesta, Messi, Mascherano, Busquets, Cuenca/Cristian Tello , Sanchez.

Chelsea: Cech Booked, Ivanovic , Cole, Cahill/Bosingwa, Terry, , Ramires, Lampard, Mikel, Meireles, Mata/Kalou, Drogba/Torres

Mabondia wanne kwenda Morocco


Kidunda
MABONDIA wanne wa  timu ya taifa ya mchezo wa ngumi inatarajia kuondoka leo kuelekea Casablanca, Morocco kushiriki michuano ya kufuzu mashindano ya olimpiki yatakayofanyika Julai mwaka huu jijini London, England.

Akizungumza jijini Dar es Salaam juzi, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Ngumi za Ridhaa Tanzania (BFT), Makore Mashaga, alisema mabondia hao wataambatana na Makamu wa Rais wa shirikisho hilo, Michael Changalawe na Kocha,  Remmy Ngabo.

Mashaga aliwataja mabondia watakaoondoka na uzito wao kwenye mabano ni Seleman Kidunda (kg 69), Abdallah Said (52), Victorian Njaiti (64) na Emilian Patrick (56).

Timu hiyo iliyokuwa imeweka kambi katika shule ya Filbert Bayi wilayani Kibaha, Pwani ilivunjwa rasmi jana.
Mashaga alisema mabondia hao watapimwa uzito  na afya Aprili 28, ambapo ufunguzi utafanyika jioni.

Katibu huyo alisema kuwa, kutokana kufungiwa kwa muda wa miaka miwili na Shirikisho la Dunia la mchezo huo (AIBA), moja ya masharti waliyopewa ni kulipa ada ya dola 750 na kutumia vifaa vyenye nembo ya Adidas.
Zuena ambaye ni mke wa Mwenyekiti mstaafu wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Kanali mstaafu Idd kipingu, alisema ni wakati wa watanzania kuungana na kujitolea kuzisaidia timu za taifa zinazoshiriki michano ya kimataifa kwa kuzisaidia mahitaji mbalimbali ili ziweze kufuzu na kuliletea sifa taifa.

Yanga hawajapata barua ya kujiuzulu wajumbe wake

Msemaji Yanga, Louis Sendeu
WAKATI timu ya Yanga ikikabiliwa na mechi dhidi ya watani wao, Simba, uongozi wa klabu hiyo umeanza kumeguka na kuwatia hofu mashabiki na wanachama  wa timu hiyo.

Yanga itaumana na Simba Mei 5, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, ukiwa ni mchezo wa mwisho wa Ligi Kuu Bara.

Akizungumza na Dira ya Mtanzania jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa klabu hiyo,  Celestine Mwesigwa, alisema mpaka hivi sasa hawana taarifa rasmi ya kujiuzulu kwa viongozi hao wawili, zaidi ya kusikia kwenye vyombo vya habari.

Katibu huyo alisema kwao itakuwa vigumu kutoa tamko kuhusu viongozi hao waliojiengua, mpaka watakapopewa taarifa rasmi.

"Kuna taratibu za kufanya kama kiongozi amejiuzulu, tukipata taarifa rasmi, tutajadili na mambo yote yatakwenda sawa," alisema Mwesigwa.

Viongozi walioripotiwa na vyombo vya habari kujiuzulu ni Seif Ahmed 'Magari' aliyekuwa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji wa klabu hiyo, kutokana nafasi hiyo alikuwa akiiwakilisha Yanga katika Kamati ya Ligi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

Magari alisema kuwa, ameamua kujiuzulu wadhifa huo kutokana na kukabiliwa na majukumu ya kifamilia, atashindwa kuitumikia vyema klabu yake, na siyo sababu za kufanya vibaya katika ligi msimu huu.

Siku moja baada ya kujiuzulu kwa Magari, mjumbe mwingine wa Kamati Ufundi, Mashindano na Usajili ya klabu hiyo, Abdallah Bin Kleb, aliwasilisha barua ya kujiuzulu nafasi yake, kutokana na na kukosa ushirikiano na uwajibikaji mbovu wa baadhi ya viongozi wa klabu hiyo.

Kumekuwa na taarifa mbalimbali zinazohusu klabu hiyo baada ya kufanya vibaya kwenye ligi hiyo, huku baadhi ya wanachama na mashabiki wakimtaka Mwenyekiti wao, Lloyd Nchunga, aachie ngazi nafasi hiyo.

Lakini, Msemaji wa klabu hiyo, Louis Sendeu, alipoulizwa kuhusu matukio hayo, alisema ni maneno ambayo yanasikika kila siku, na ikifika wakati wataweka wazi kila kitakachokuwa kikitokea ikiwa pamoja na kujiuzulu kwa viongozi hao.

Tuesday, April 24, 2012

BIN KLEB: ILIKUWA NIONDOKE NA MOSHA


Bin Kleb kushoto, akimkabidhi Niyonzima jezi baada ya kumsainisha mwaka jana Kigali, rwanda

MJUMBE wa Kamati ya Mashindano ya klabu ya Yanga, Abdallah Ahmed Bin Kleb amesema kwamba ilikuwa ajiuzulu siku nyingi, baada ya Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo, Davis Mosha kujiuzulu, Machi mwaka jana.
Akizungumza na bongostaz.blogspot.com, Bin Kleb alisema kwamba amekuwa akivumilia mambo mengi ya uongozi, alkini imefikia wakati anaamua kujiweka pembeni.
“Ilikuwa niondoke muda mrefu tu tangu wakati ule Mosha alipojiuzulu, lakini nikavuta subira, ila kwa sasa nimefikia mwisho.
Bin Kleb na Jumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga, Seif Ahmad ‘Magari’, ambaye ni swahiba wake kipenzi wamewasilisha barua za kujiuzulu wadhifa wao huo wa kuteuliwa.
Mwenyekiti wa Yanga, Wakili Lloyd Baharagu Nchunga ameiambia bongostaz.blogspot.com mchana huu kwamba, ameambiwa juu ya Wajumbe hao wa Kamati ya Mashindano, kuwasilisha barua za kujiuzulu.
Alipoulizwa sababu zilizoainishwa na watu hao kwenye barua zao, Nchunga alisema kwamba ni kutokuwana imani na uongozi.
“Alipokuwa akizungumza na Radio One jana, alisema ni kwa sababu za kifamilia, lakini katika barua niliyosomewa na Katibu (wa Yanga, Celestine Mwesigwa), Seif amesema haridhishwi na mambo yanavyokwenda kwenye  uongozi,”alisemsa Nchunga akiinukuu barua ya Seif.
“Anasema hapati taarifa za fedha kutoka kwa Katibu. Anasema fedha nyingi zinaingia Yanga, lakini yeye hajulishwi, wakati wao wanatumia fedha nyingi kugharamia klabu,”alisema Nchunga.
Nchunga alisema yeye alikuwa safarini Afrika Kusini na amerejea jana, lakini hajaziona rasmi hizo barua bali amesomewa na Katibu Mkuu.
Lakini alipoulizwa maoni yake juu ya madai ya Seif, kwanza Nchunga alisema; “Kwanza nataka niseme, huu haukuwa wakati mwafaka kuleta haya mambo, tuna wiki mbili kabla ya kucheza na Simba. Hizi ni dalili mbaya,”alisema.
Kuhusu madai ya Seif kutojulishwa taarifa za fedha, Nchunga alisema kwamba taarifa za fedha zinatolewa katika vikao vya Kamati ya Utendaji.
“Na sisi tunakutana sana, na kama mtu anataka kuhoji jambo, hakatazwi, sasa sielewei hii inatoka wapi,”alisema.
Lakini Nchunga alisema inawezekana matokeo mabaya msimu huu yamechafua hali ya hewa ndani ya Yanga kiasi kwamba viongozi hao wameshindwa kuimudu.
“Kuna mengi katika wakati huu timu ikiwa vibaya, kuna kuzongwa na wanachama na nini, ni mambo ambayo viongozi wanatakiwa kuvumilia na tujipange upya kwa ajili ya mashindano yajayo, lakini si kujiuzulu,”alisema Nchunga.
Pamoja na hayo, Nchunga alisema kwamba anawatafuta kwanza viongozi hao azungumze nao na kujaribu kuwashawishi warudi katika uongozi.
“Nina wajibu wa kufanya jitihada za haraka ili kunusuru mmomonyoko huu usitokee, huu ni wakati ambao wana Yanga tunapaswa kushikamana sana ili kuinusuru klabu yetu, hapa ninatoka kuanza kuhangaikia hilo,”alisema Nchunga.
Yanga ipo katika wakati mgumu hivi sasa, baada ya kukosa nafasi ya kucheza ya michuano ya Afrika mwakani, ikizidiwa kete na Azam FC.
Yanga ilipoteza nafasi hiyo, baada ya kupoteza pointi tisa mfulilizo katika mechi dhidi ya Coastal Union, Toto African na Kagera Sugar.
Pamoja na kuifunga Coastal bao 1-0, lakini Yanga ilipokonywa pointi kwa kosa la kumtumia beki Nadir Haroub ‘Cannavaro’ akiwa anatumikia adhabu kabla ya kwenda kufungwa 3-2 na Toto na 1-0 na Kagera.
Seif na Bin Kleb ni watu muhimu mno ndani ya Yanga kwa sasa, ambao wazi kama wataachia ngazi klabu itayumba na kuna hatari ya kupoteza malengo ya msimu ujao.
Achilia mbali ujanja wao wa mjini unaowawezesha kupambana na fitina za wapinzani wao katika Ligi Kuu, lakini wamekuwa wakihudumia timu kuanzia usajili na uendeshaji.
 
 (kwa msaada wa Bin Zubeiry)

Wasanii kizazi kipya wapewa darasa

Che Mundugwao (kushot0)
WASAANI wa muziki wa kizazi kipya wameshauriwa kuwa na msimamo katika aina ya mahadhi ya muziki wanaoimba kuliko ilivyo sasa, ambapo huchanganya na kushindwa kueleweka.

Wito huo umetolewa wiki hii na wadau wa sanaa katika Jukwaa la Sanaa linalofanyika kila wiki makao makuu ya Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA).

Wadau wa wasanaa walisema kuwa, hali hiyo imeufanya muziki nchini ukose utambulisho na kushindwa kufanya vizuri kimataifa.

"Wasanii wetu huchanganya mahadhi (aina) ya muziki wanaoimba, leo ataimba reggae, kesho zouk mara muziki wa asili, hii inamfanya msanii asieleweke aina ya muziki anaoimba, lakini pia tunakosa ubobezi kwenye aina hizi," alisema Che Mundugwao ambaye ni Makamu wa Rais wa Shirikisho la Muziki Tanzania.

Alisema kuwa, kubadilika kwa wasanii kwenye aina ya muziki wanaoufanya, kumeufanya muziki wetu ushindwe kuvuma kimataifa na kukosa utambulisho kwenye aina nyingine za muziki unaopatikana na kufahamika duniani kote.

"Muziki ni lugha ya dunia, aina zake zinafahamika duniani kote, tunachopaswa kufanya ni kutumia vionjo vya asili yetu ili kuleta utofauti. Tusipofanya hivyo tutaendelea kuwatumbuiza watanzaia wenzetu waishio ughaibuni tu na si kufanya matamasha ya kimataifa," alisistiza Che Mundugwao ambaye pia ni msanii wa muziki wa asili.

Mdau mwingine aliyefahamika kwa jina la Mbile Hango alionya kuwa, wasanii wetu wataendelea kuvuma kwa muda mfupi na kutoweka kama hawatazingatia taaluma na ubobezi katika aina fulani ya muziki.

Aliongeza kuwa, ni vigumu kwa wasanii kuimba kwa kunakiri muziki kutoka nchi za nje kama ile ya kwaito yenye asili ya Afrika Kusini na kutegemee kupata fursa ya kuuza kazi zao nje na kushiriki matamasha ya kimataifa.

"Ukinakiri muziki kutoka nje, maana yake huna kipya cha kupeleka nje, tutaendelea kuvuma humu humu ndani," alisema.

Mjadala wa wiki hii kwenye Jukwaa la Sanaa ulijikita kwenye Ubora katika Utunzi wa Tungo za Muziki

WATANZANIA KUCHEZESHA AFRIKA KUSINI


Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limewateua waamuzi wane wa Tanzania kuchezesha mechi ya marudiano ya 16 bora ya Kombe la Shirikisho kati ya Black Leopards ya Afrika Kusini na Warri Wolves ya Nigeria itakayochezwa nchini Afrika Kusini kati ya Mei 4, 5 na 6 mwaka huu.
 
Waamuzi hao ni Waziri Sheha atakayepuliza filimbi wakati wasaidizi wake watakuwa John Kanyenye na Erasmo Jesse. Mwamuzi wa akiba (fourth official) atakuwa Israel Mujuni. Kamishna wa mechi hiyo atakuwa Aurelio Mathias wa Msumbiji.
 
Mechi ya kwanza kati ya timu hizo itachezwa Jumapili (Aprili 29 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Warri City ulioko Jimbo la Delta nchini Nigeria na itachezeshwa na waamuzi kutoka Senegal wakati Kamishna atakuwa Inyangi Bokinda wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC).

POLISI MORO, MGAMBO, PRISONS ZAPANDA VPL


Boniface Wambura
Fainali ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL) iliyoshirikisha timu tisa imemalizika jana (Aprili 23 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro huku tatu zikifuzu kucheza Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) msimu wa 2012/2013 utakaonza Agosti mwaka huu.
 
Akizungumza Dar es Salaam leo, Msemaji wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Boniface wambura, alizitaja timu hizo ni Polisi Morogoro iliyofikisha pointi 20 ikifuatiwa na Mgambo Shooting ya Tanga (15) na Tanzania Prisons ya Mbeya iliyomaliza katika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 14.
 
Nyingine zilizofuatia na pointi zao kwenye mabano ni Polisi Dar es Salaam (13), Mbeya City Council (11), Rhino Rangers ya Tabora (8), Mlale JKT ya Ruvuma (8), Polisi Tabora (6) na Transit Camp ya Dar es Salaam (2).

YANGA, POLISI DODOMA ZAAMBULIA SH193,858.47


Mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom kati ya Yanga na Polisi Dodoma iliyochezwa (Aprili 22 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ilishuhudiwa na watazamaji 1,635 na kuingiza sh. 5,666,000.
 
Baada ya kuondoa gharama za awali za mchezo na asilimia 18 ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ambayo ni sh. 864,305.08 kila klabu ilipata sh. 193,858.47, uwanja sh. 26,469.49.
 
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) sh. 26,469.49, Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 108,687.80. Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 13,234.75, Baraza la Michezo la Taifa (BMT) sh. 2,646.95 na asilimia 10 ya gharama za mechi ni sh. 26,469.49.
 
Gharama za awali za mechi zilikuwa nauli ya ndani kwa waamuzi sh. 10,000, nauli ya ndani kwa kamishna wa mchezo sh. 10,000. Mwamuzi wa akiba sh. 30,000, posho ya kujikimu kwa kamishna na waamuzi sh. 160,000, gharama ya tiketi sh. 1,500,000, usafi na ulinzi kwa uwanja sh. 1,500,000 na Wachina (Beijing Construction) sh. 1,000,000.
 
Kutokana na mechi hiyo kuingiza kiasi kidogo baadhi ya gharama zililipwa nusu au kutolipwa kabisa na kuacha madeni. Madeni hayo ni tiketi sh. 1,500,000, maandalizi ya uwanja (pitch marking) sh. 400,000, umeme sh. 300,000, usafi na ulinzi kwa uwanja sh. 850,000 na Wachina sh. 1,000,000.

SIMBA, MORO UNITED ZAINGIZA MIL 28/-

Mzambia Felix Sunzu, akishangilia baada ya kufunga bao.
Pambano la Ligi Kuu ya Vodacom kati ya Simba na Moro United lililochezwa jana (Aprili 23 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam limeingiza sh. 28,688,000.
 
Jumla ya watazamaji 7,945 walikata tiketi kushuhudia mechi hiyo kwa viingilio vya sh. 3,000, sh. 5,000, sh. 10,000 na sh. 15,000. Watazamaji 6,946 kati ya hao walishuhudia mechi hiyo kwa kiingilio cha sh. 3,000.
 
Baada ya kuondoa gharama za awali za mchezo na asilimia 18 ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ambayo ni sh. 4,376,135.59 kila klabu ilipata sh. 4,919,009.32, uwanja sh. 1,454,286.44.
 
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) sh. 1,454,286.44, Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 1,058,414.58, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 727,143.22, Baraza la Michezo la Taifa (BMT) sh. 145,428.64 na asilimia 10 ya gharama za mechi ni sh. 1,454,286.44.
 
Gharama za awali za mechi zilikuwa nauli ya ndani kwa waamuzi sh. 10,000, nauli ya ndani kwa kamishna wa mchezo sh. 10,000, mwamuzi wa akiba sh. 30,000, posho ya kujikimu kwa kamishna na waamuzi sh. 80,000, gharama ya tiketi sh. 3,000,000, maandalizi ya uwanja (pitch) sh. 400,000, umeme sh. 300,000, usafi na ulinzi kwa uwanja sh. 2,350,000 na Wachina (Beijing Construction) sh. 2,000,000.
 
Nayo mechi kati ya Villa Squad na African Lyon iliyochezwa Aprili 22 mwaka huu kwenye Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam iliingiza sh. 496,000 ambapo kila klabu ilipata sh. 68,061.70 wakati watazamaji walioshuhudia mechi hiyo ni 469.
 
Vilevile mechi kati ya Tanzania (Ngorongoro Heroes) na Sudan iliyochezwa Aprili 21 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam iliingiza sh. 9,717,000 kutokana na washabiki 2,562.

Monday, April 23, 2012

LULU MAHAKAMANI LEO, WAANDISHI WAZUIWA KUMPIGA PICHA

Mtuhumiwa wa mauaji ya mwigizaji Steven Charles Kanumba, Elizabeth Michael 'Lulu' akiingia Mahakama ya Kisutu kwa ajili ya kesi yake leo, chini ya ulinzi mkali wa askari wa Magereza, ambao walikuwa wanawazuia Waandishi wa habari kupiga picha.

YANGA YAOMBA RADHI MKUTANO MKUU

Mohamed Bhinda

Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga ambaye pia mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF akiwakilisha klabu za Mkoa wa Dar es Salaam, Mohamed Bhinda aliwaomba radhi wajumbe wa Mkutano Mkuu kwa kitendo cha wachezaji wake kumpiga mwamuzi Israel Nkongo kwenye mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom dhidi ya Azam iliyochezwa Machi 10 mwaka huu.
 
Pia alimuomba Rais wa TFF, Leodegar Tenga kutoa msamaha wa adhabu ya kulipa faini iliyotolewa na Kamati ya Ligi ya TFF kwa wachezaji wawili wa Yanga ambao mpaka sasa hawajalipa faini hiyo.
 
Rais Tenga alimshukuru Bhinda kwa ujasiri alioonesha wa kuomba radhi mbele ya wajumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF kwa kitendo kile. Aliongeza kuwa kwa vile yeye ni muumini wa kanuni, na adhabu hizo zimetolewa kwa mujibu wa kanuni hawezi kutoa msamaha, hivyo wachezaji hao walipe faini hizo.
 
Pia Rais Tenga alisema binafsi haziingilia kamati za TFF katika uamuzi ambao zinafanya kwa vile zina watu waadilifu, na angekuwa yeye binafsi ndiye anayetoa adhabu, angetoa adhabu kali zaidi kwa vile vitendo vya kupiga waamuzi havikubaliki katika mchezo wa mpira wa miguu.

KANUNI ZA NIDHAMU, MAHAKAMA YA USULUHISHI

Tenga
Akizungumza wakati wa kufunga mkutano huo, Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga, aliwaambia wajumbe kuwa Kanuni za Nidhamu (Disciplinary Code) za TFF na uundaji wa Mahakama ya Usuluhishi (Arbitration Tribunal) ya TFF ambacho ndicho kitakuwa chombo cha juu cha kutoa haki kwa masuala ya mpira wa miguu nchini vitakamilika mwaka huu.
 
Pia TFF itaendelea kutafuta wadhamini kwa ajili ya timu za Taifa za vijana na wanawake, itaendelea kuendesha semina na makongamano katika nyanja mbalimbali za mpira wa miguu, kutengeneza mtaala wa academy na kutengeneza mpango wa maendeleo (Comprehensive Plan) baada ya ule wa awali kumalizika mwaka huu.

MKUTANO MKUU WA MWAKA 2011 WA TFF

Wambura

Mkutano Mkuu wa Mwaka (AGM) wa 2011 wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) umefanyika kwa siku mbili (Aprili 21-22 mwaka huu) kwenye ukumbi wa NSSF Waterfront na kuhudhuriwa na wajumbe 104. Mkutano ulipokea taarifa, kufanya uamuzi katika masuala mbalimbali na mengine yaliyojitokeza kama ifuatavyo;
 
EL MAAMRY, NDOLANGA WATUNUKIWA URAIS WA HESHIMA
AGM ilipitisha pendekezo la kuwatunuku urais wa heshima wa TFF, Alhaji Said Hamad El Maamry na Muhidin Ahamadi Ndolanga lililowasilishwa na Mwenyekiti wa mkutano huo ambaye pia ni Rais wa TFF, Leodegar Tenga.
 
Alhaji El Maamry ambaye ni mjumbe wa heshima wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) alikuwa Mwenyekiti wa TFF wakati huo ikiitwa Chama cha Mpira wa Miguu Tanzania (FAT) kuanzia mwaka 1973 hadi 1986. Alhaji Ndolanga aliongoza FAT kuanzia mwaka 1993 hadi 2004.
 
BAJETI YA MWAKA 2012
Bajeti ya Mwaka 2012 ya sh. 7,246,628,650 kwa ajili ya matumizi ya TFF ilipitishwa. Kwa mwaka 2012 TFF inatarajia kukusanya sh. 7,572,991,433 kupitia vyanzo mbalimbali.
 
Vyanzo hivyo ni viingilio vya uwanjani vinavyotarajiwa kuingiza asilimia 22 ya mapato yote, udhamini (asilimia 74) na vyanzo vingine kama haki za matangazo ya televisheni, ada za ushiriki wa timu katika mashindano mbalimbali, misaada kutoka FIFA na CAF ambayo kwa pamoja vinatarajiwa kuingiza asilimia nne ya mapato yote.
 
KAMATI YA LIGI YA TFF
Kamati ya Ligi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) itaendelea na mchakato wa kupendekeza mifumo mitatu tofauti ya chombo kitakachosimamia/kuendesha Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) na Ligi Daraja la Kwanza (FDL) ikieleza faida na athari za kila mfumo uliopendekezwa na baadaye kuwafanya mawasilisho (presentation) kwenye Kamati ya Utendaji.
 
Baada ya kuwasilisha mifumo hiyo kwa Kamati ya Utendaji, Kamati ya Ligi itapendekeza mfumo upi kati yao hiyo inaoona unafaa kabla ya kufanyika uamuzi wa mwisho.
 
Lengo la kuunda chombo maalumu cha kuendesha ligi ni kuongeza ufanishi katika uendeshaji wa VPL na FDL, na pia kuifanya Sekretarieti ya TFF kushughulikia zaidi shughuli za maendeleo.
 
UUZWAJI WA TIMU
Uuzaji wa timu linabaki kuwa suala la kisheria. Lakini TFF imeweka utaratibu ufuatao; lazima Mkutano Mkuu wa klabu husika uidhinishe uuzaji, na timu ikishauzwa inabaki katika mkoa husika.
 
MFUMO WA MASHINDANO
Kwa vile kuna tatizo la ligi mbalimbali kuwa fupi, hali inayosababisha baadhi ya wachezaji katika madaraja ya chini kucheza ligi zaidi ya moja katika msimu mmoja, mfumo wa ligi/mashindano utaangaliwa upya.
 
Mfumo uliopo sasa uliwekwa kwa ajili ya kuvutia uwekezaji katika mpira wa miguu ambapo mwekezaji anaweza kuanzisha timu, na ndani ya miaka mitatu ikacheza Ligi Kuu. Pili, ilikuwa ni kuondoa mlolongo mrefu wa ligi, na kuwafanya wanachama wa TFF (mikoa) nao kuendesha ligi zao mikoani.
 
Ijulikane kuwa ligi za mikoa (regional leagues) zinachezwa. Kwa sababu TFF inaendeshwa kwa mfumo wa shirikisho (federation), nia ni wanachama wa federation nao kuwa na majukumu ya kusimamia na kuendesha ligi, kwa vile TFF haiwezi kusimamia ligi zote.
 
MAREKEBISHO YA KATIBA
Mkutano Mkuu wa TFF umepitisha marekebisho ya Katiba katika maeneo mawili; moja ni kuanzisha Baraza la Wadhamini ambalo linatakiwa kuwa na wajumbe wasiopungua watatu na wasiozidi watano.
 
Marekebisho mengine ni kuongeza idadi ya kanda kutoka kumi na moja za sasa hadi 13. Marekebisho hayo yamefanyika kutokana na Serikali kuongeza mikoa mipya ya kijiografia.
 
Kanda mpya sasa zitakuwa Kagera/Geita, Arusha/Manyara, Kilimanjaro/Tanga, Katavi/Rukwa, Njombe/Ruvuma, Dodoma/Singida, Dar es Salaam, Shinyanga/Simiyu, Mwanza/Mara, Lindi/Mtwara, Kigoma/Tabora, Mbeya/Iringa na Pwani/Morogoro.
 
Ukiondoa mamlaka ya uteuzi aliyonayo Rais kwa mujibu wa Katiba ya TFF, wajumbe wote wa Kamati ya Utendaji huchaguliwa kwa kanda.
 
HESABU ZILIZOKAGULIWA
Mkutano Mkuu ulipitisha hesabu zilizokaguliwa za mwaka 2010 (Audited Accounts) , na pia kuiteua kampuni ya ukaguzi wa hesabu ya TAC Associates kuwa mkaguzi wa hesabu za TFF kwa kipindi cha miaka minne ijayo.